Skip to main content
Na Sparrow Daviceous: OFISI ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa (Tamisemi), imewaandikia baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji barua za kuwabadilishia majukumu, baada ya kubainika wameshindwa kwenda na kasi ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari. Katibu Mkuu wa Tamisemi, Jumanne Sagini, alitoa taarifa hiyo hivi karibuni mjini Dodoma wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha kupitia kanuni na mwongozo wa uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa. “ Baadhi ya wakurugenzi wameandikiwa barua za kupewa majukumu mengine baada ya kubainika kuwa kasi yao katika ujenzi wa maabara tatu hauendi kwa kasi,” alisema Sagini. Alisisitiza, “Hatutakuwa na huruma kwa suala hili la ujenzi wa maabara tatu ...Tamisemi haipendi kumpoteza mkurugenzi hata mmoja ifikapo Desemba 9 mwaka huu.” Alisema, pamoja na shughuli za uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu, suala la ujenzi wa maabara tatu bado lipo pale pale kama lilivyo pangwa na halina mjadala mwingine, isipokuwa kukamilishwa katika muda uliopangwa. “ Maabara si mchezo, wakurugenzi jitahidini, lazima maabara zikamilishwe , kwani suala hilo si la mchezo , hakuna cha kukwepa ,“ alisema. Alisema, “kila mmoja akitoka hapa kwenye kikao hiki, ajue kuwa moja ya majukumu yake licha ya kusimamia na uendeshaji wa uchaguzi huu, ni kukamilisha ujenzi wa maabara tatu ili kila mmoja wetu abaki salama katika ajira yake.
Comments
Post a Comment